Moja kati ya vitu vigumu maishani, ni kuishi kama
unavyotaka wewe maisha yawe.
Mara kwa mara utajikuta unachanganywa na vitegemezi kama chakula,
manunuzi, matukio ya televisheni, mitandao ya kijamii na hata simu za mkononi.
Vitegemezi hivi vinachangia kukuondoa katika uhalisia wako wa
maisha na kukusahaulisha hisia za kweli na unajikuta unapoteza fursa zilizopo.
Unapokuwa mpweke ndio unapata muda wa kuzitafakari hisia zako
halisi kwa kina:
uoga, hofu, furaha, hasira, au hata huzuni.
Haijalishi hisia zako ni hasi au chanya lakini zinakupa picha
halisi ya unataka nini katika maisha.
Tuangalie kwa pamoja sababu zinazochangia
mpaka unapoteza fursa zilizopo:
1.KUTAKA KUFANYA KILA KITU:
Karibu kila binadamu kuna kipindi anahisi anapitwa na vitu
vinavyofanyika duniani, ambavyo anatamani pia angekuwa anavifanya.
Lakini hakika unaweza ukazunguka kila sehemu na kutaka kujihusisha
na kila kitu, mathalani kufanya kazi,au burudani masaa 24 bila
kulala lakini bado hautaweza kujihusisha na kila kitu.
Kwahiyo achana na hisia za kwamba unapitwa na mambo na tambua kila
unachotakiwa kufanya kipo katika mazingira yako.
2.KUKWEPA MAUMIVU NA KUSHINDWA:
Usijaribu kuukimbia ukweli wa maisha yanayokukabili, kwani maumivu
na kushindwa ndio vitu vinavyosaidia ukuaji wako wa akili.
Kumbuka, kuna tofauti kati ya kuwa katika mazingira ya kushindwa
na kuwa umeshindwa tayari .
Hautaweza kuvikimbia vitu hivi mpaka viwe vimekufundisha
unachopaswa kukijua katika maisha yako, ili uchukue hatua nyingine mbele.
3.KUENDELEA KUSHIKILIA KUMBUKUMBU ZA ZAMANI:
Usijaribu kutumia muda wako mwingi kufikiria mambo mabaya ambayo
yalishapita kwani kufanya hivyo ni kuyaruhusu yaharibu wakati uliopo.
Usijaribu kuishi wakati mwengine, unatakiwa ukubali kumaliza hizo
kumbukumbu ili uanze kujenga mwanzo mpya.
Anza kufunga kumbukumbu za mambo mabaya ya zamani sasa na jua
hayatakuongoza unapotaka kufika.
4.KUJIKUMBUSHIA MATUKIO YA KUSHINDWA:
Kama ukiendelea kujisimulia historia za matukio uliyoshindwa
kichwani mwako, utayaamini na kujiona ni mtu wa kushindwa daima.
Swali ni: Historia unayojisimulia inakutia nguvu?
Usiendelee kuweka makosa yako kichwani, kwani uzito wake
utaangusha uwezo wako halisi.
Unapaswa utambue kuwa kila kitu mwanzo huwa ni kigumu kabla
hakijawa rahisi.
5.KUIGIZA MAISHA YA MWENGINE:
Vita kali zaidi uliyowahi kupigana nayo ni vita ya kutaka kuwa
wewe, hivyo ulivyo sasa.
Hautawezi kuwa wewe kama kila siku unajitafuta kwa watu wengine.
Kumbuka, unapoigiza maisha ya mtu mwengine unapoteza nafasi ya
kujitumia wewe mwenyewe na uwezo wako wa asili utakufa kwa kuwa hautumiki.
6.PICHA YAKO KICHWANI YA UNAVYOTAKA VITU VIWE:
Moja kati ya vitu vinavyokuangusha katika maisha ni picha
unayoijenga kichwani
na kutaka kila kitu kiwe kama ulivyokiona wewe mawazoni.
Maisha yanasonga na mara kwa mara sio kama ulivyotaka yawe, bali
kadri yalivyopaswa yawe.
Maisha ni kama muziki unaochezwa ambao haukuuchagua, lakini
unaweza ukachagua namna ya kuucheza.
7.KUJIONA UNA KASORO:
Usijihukumu mwenyewe, kuna watu wengi wanatamani kufanya hiyo kazi
kwa ajili yako.
Fanya unayopaswa kufanya kwa uwezo wako na mengine yanayobaki
yasalimishe kwa wengine.
Jipende na jionee fahari na kila kitu unachofanya hata kama
umekosea kwani hata makosa yanaonyesha ulijaribu kufanya.
8.KUENDELEA KUSUBIRI:
Acha kuendelea kuisubiri kesho, kwani muda wa leo hautaupata tena.
Maisha ni mafupi sana kama kila siku unaomba udhuru.
Achana na mitazamo ya kutaka kufanya kila kitu kesho, anza leo
kufanya hatua japo moja ya jambo lako kwa ujasiri.
Kama huna hakika ni njia gani hasa unayopaswa kupita, kufuata moyo
wako ndio njia bora iliyobaki.
KAA TAFAKARI NI JAMBO LIPI KATI HAYO HAPO JUU LIMEKUWA TATIZO KWA
WEWE KUFIKIA MALENGO YAKO.
ANZA KULISHUGHULIKIA SASA NA UTAONA MATUNDA YAKE.
No comments:
Post a Comment