Sehemu ya wazee wa Mkoa Dar es Salaam wakishangilia kuunga mkono kufukuzwa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maenedeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka jana. Picha na Venance Nestory .
Hotuba ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow imepokewa kwa
hisia tofauti na wasomi, wanasiasa na wananchi wa kawaida, wengi wakionyesha kutoridhishwa na hatua alizochukua.
hisia tofauti na wasomi, wanasiasa na wananchi wa kawaida, wengi wakionyesha kutoridhishwa na hatua alizochukua.
Akizungumza kwa simu baada ya hotuba hiyo Jana Desemba 22,2014, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema:- kitendo chake cha kuwatetea waliohusika katika kashfa hiyo ya uchotwaji wa Sh306 bilioni kitakigharimu chama chake cha CCM siku chache zijazo.
Alisema kuachwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakimu Maswi si cha kupongezwa kwa sababu viongozi hao ndiyo wahusika wakuu wa kashfa hiyo.
“Ameonyesha kuwa kazi iliyofanywa na Bunge, ikiwahusisha mawaziri aliowateua waliotumia uchunguzi uliofanywa na vyombo vya Serikali ni bure kabisa. Hotuba yake ina maana kuwa uchunguzi wa Ikulu ndiyo unaotakiwa kuaminika.”
Huku akionyesha kukerwa na jinsi Rais Kikwete alivyokuwa akiyarudiarudia maazimio ya Bunge, Mbowe alisema katika hotuba yake, Rais Kikwete amekiri kuwa miamala yote ya fedha iliyofanyika katika benki ilikuwa halali, kitu ambacho si kweli.
“Profesa Tibaijuka ametolewa kafara tu. Huyu alikuwa katika tawi tu la kashfa ya escrow, wahusika wakuu walikuwa ni Muhongo na Maswi ila wameachwa. Rais anatetea watu badala ya kuwachukulia hatua. Hakika anazidi kuchochea moto,” alisema.
Aliongeza, “Tunaitakia CCM maisha marefu na Rais Kikwete ili siku moja waje waone jinsi kauli ya Rais kuhusu escrow itakavyoitafuna CCM. Inakuwaje Rais anashindwa kusoma hisia za Taifa juu ya jambo hili?”
Wakati Mbowe akieleza hayo, wasomi mbalimbali nchini wamepongeza hatua iliyochukuliwa na Rais Kikwete huku wakiwashauri viongozi waliotajwa katika maazimio ya Bunge kwamba mamlaka za uteuzi ziwawajibishe, wajiuzulu wenyewe kabla ya majibu ya uchunguzi dhidi yao hayajatoka.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kauli,- hotuba na hatua za Rais Kikwete ni kuwapaka Watanzania mafuta kwa mgongo wa chupa.
“Kimaadili, viongozi wote waliotajwa kuhusika kwenye sakata la escrow walipaswa kujiuzulu. Rais alistahili kuwaagiza waachie ngazi na wasipofanya hivyo, awawajibishe. Siyo kupaka watu mafuta kwa mgongo wa chupa kama alivyofanya kwenye hotuba yake.”
Alisema Taifa liko katika hali tete, huku wahisani wakisimamisha misaada ya kimaendeleo, lakini Rais haonekani kuchukua hatua madhubuti siyo tu kurejesha imani ya wananchi na wahisani kwa Serikali, bali kunusuru nchi.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema,- “Nimemsikiliza Rais, ninachoweza kusema ni kwamba maazimio yale hayakuwa ya Zitto Kabwe, PAC, CAG au PCCB. Yalikuwa ni ya Bunge zima. Bunge la vyama vyote kikiwamo chama cha Rais Kikwete yaani CCM.
“Sisi kama Bunge tulitoa maazimio yale kwa maridhiano, uzalendo na bila kutaka kumwonea mtu yeyote. Suala hili sasa naliacha kwa wananchi. Bunge limefanya kazi yake na Serikali ambayo ndiyo tulikuwa tunasubiri maamuzi yake imeamua hivyo. Wananchi wataamua wenyewe,” alisema.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), aliyeibua sakata la escrow bungeni, David Kafulila alisema:- “Rais amekwepa majukumu yake katika kuwachukulia hatua wahusika. Maazimio ya Bunge yalitaka mamlaka ya uteuzi ichukue hatua dhidi ya mawaziri, yeye ndiye aliyewateua iweje amwache Profesa Muhongo?”
Alisema Rais Kikwete alitengua uteuzi wa mawaziri waliong’olewa kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza na kuagiza uchunguzi ufanywe dhidi yao, huku akihoji iweje kwa Profesa Muhongo uchunguzi ufanyike huku akiwa bado waziri.
“Rais anasema fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow zilitolewa kwa amri ya Mahakama, sasa iweje fedha zitolewe wakati bado kulikuwa na mvutano kati ya Tanesco na IPTL, ambao katika hotuba yake pia amekiri kuwa ulikuwepo?” alisema.
Kafulila pia aliponda kitendo cha Rais Kikwete kusema kutaifisha mitambo ya IPTL ni kukimbiza wawekezaji, wakati tayari amekiri kuwa suala la IPTL na PAP lina utata mkubwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema:- “Rais amejitahidi kufafanua suala hili, hasa juu ya fedha za escrow ni za Serikali au IPTL na kuhakikisha utawala wa kisheria unafanya kazi ipasavyo kulingana na maazimio ya Bunge.”
Kuhusu Profesa Tibaijuka, Dk Bana alisema uamuzi uliochukuliwa dhidi yake ni sahihi kwa sababu alipewa fedha kupitia akaunti yake binafsi na kwamba kitendo chake cha kukanusha kuhusika na suala hilo kupitia vyombo vya habari pia kilimponza.
Profesa Kitila Mkumbo wa UDSM alisema:- “Profesa Muhongo anatakiwa kuachia ngazi. Kauli ya Rais kwamba ‘anamweka kiporo’ maana yake anamtaka ajiuzulu bila aibu kama iliyomkuta Profesa Tibaijuka. Rais hakuyadharau maazimio ya Bunge kama viongozi wengine walivyoyadharau. Wote waliotajwa katika ripoti ile wanatakiwa kuachia ngazi na si kusubiri mpaka kutimuliwa.”
Profesa wa Chuo Kikuu Ruaha, Gaudence Mpangala alisema:- “Maamuzi yake hayakutarajiwa na wananchi, ripoti ya uchunguzi ya CAG imebainisha kuwa fedha za escrow ni za umma, sasa kama ni za IPTL uchunguzi wa nini?”
No comments:
Post a Comment